Alhamisi, 23 Oktoba 2014

Taarifa kutoka Kaskazini Mashariki mwa Nigeria,
zinasema kuwa idadi kubwa ya wanawake wengine
wametekwa nyara na kundi la wapiganaji la Boko
Haram.
Wiki jana maafisa wakuu wa nchi hiyo walitangaza
kufikia makubaliano ya kusitisha vita na kundi hilo.
Kwa hiyo kundi hilo lilikubali kuwaachilia wasichana
zaidi ya mia mbili waliotekwa na kundi hilo kama
sehemu ya makubaliano hayo miezi sita iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo
hilo, wapiganaji wa Boko Haram walishambulia vijiji
viwili katika jimbo la Adamawa - Waga Mangoro na
Garta.
Kisha wakawateka wasichana na wanawake wengi.
Vijiji hivi vinapakana na miji ya Madagali na Michika
ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa wapiganaji
hao kwa wiki kadhaa.
Kundi la kwanza la wasichana wlaiotekwa nyara
na Boko Haram ambao bado kuachiliwa
Mashambulizi hayo yalifanyika Jumamosi siku moja
tu baada ya jeshi la Nigeria kutangaza makubaliano
ya kusitisha vita kuwa yamefikiwa kati ya serikali
na Boko Haram.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, serikali
ilisema wasichana 219 waliotekwa kutoka Chibok
mwezi Aprili, wataachiliwa hivi karibuni.
Tangu tangazo hilo kutolewa, kundi hilo limeendelea
kufanya mashambulizi, na hapajakuwa na kauli
yoyote ikiwa wasichana wa Chibok wameachiliwa.
Kulingana na serikali, mazungumzo yalitarajiwa
kufanyika kati ya serikali na Boko Haram, wiki hii
nchini Chad.
Wakati huo huo, polisi wanasema kuwa shambulizi
lililofanywa katika jimbo la Bauchi liliwaua watu
watano.
Mashambulizi yoyote yanayofanywa kaskazini mwa
Nigeria hulaumiwa kundi la Boko Haram. Hata hivyo
kundi hilo kwa kawaida halijibu haraka na kwa
hivyo huwa vigumu kuthibitisha ukweli kama ni
wapiganaji hao waliofanya mashambulizi hayo au
la.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni